Nambari SURA YA 1 1 Bwana akanena na Musa katika bara ya Sinai, ndani ya hema ya kukutania, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, mwaka wa pili baada ya kutoka kwao katika nchi ya Misri, akamwambia, 2 Fanyeni jumla ya mkutano wote wa wana wa Israeli, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, na hesabu ya majina yao, kila mwanamume kwa kichwa; 3 tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote wawezao kwenda vitani katika Israeli; wewe na Haruni mtawahesabu kwa majeshi yao. 4 Na mtu mume wa kila kabila atakuwa pamoja nanyi; kila mtu mkuu wa mbari ya baba zake. 5 Na majina ya wanaume watakaosimama pamoja nanyi ni haya: kabila ya Reubeni; Elisuri mwana wa Shedeuri. 6 wa Simeoni; Shelumieli mwana wa Suri-shadai. 7 Wa Yuda; Nashoni mwana wa Aminadabu. 8 wa Isakari; Nethaneli mwana wa Suari. 9 wa Zabuloni; Eliabu mwana wa Heloni. 10 Wa wana wa Yusufu; wa Efraimu; Elishama mwana wa Amihudi; wa Manase; Gamalieli mwana wa Pedasuri. 11 wa Benyamini; Abidani mwana wa Gideoni. 12 wa Dani; Ahiezeri mwana wa Amishadai. 13 wa Asheri; Pagieli mwana wa Okrani. 14 wa Gadi; Eliasafu mwana wa Deueli. 15 wa Naftali; Ahira mwana wa Enani. 16 Hao ndio waliotajwa katika mkutano, wakuu wa kabila za baba zao, wakuu wa maelfu katika Israeli. 17 Musa na Haruni wakawatwaa watu hawa waliotajwa majina yao; 18 Nao wakakutanisha mkutano wote siku ya kwanza ya mwezi wa pili, nao wakaandika vizazi vyao kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wakuu wao. 19 Kama Bwana alivyomwagiza Musa, ndivyo alivyowahesabu katika jangwa la Sinai. 20 Na wana wa Reubeni, mwana mkubwa wa Israeli, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, vichwa vyao, kila mwanamume tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 21 wale waliohesabiwa katika kabila ya Reubeni, walikuwa arobaini na sita elfu na mia tano. 22 Katika wana wa Simeoni, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya majina, vichwa vyao, kila mwanamume tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 23 wale waliohesabiwa katika kabila ya Simeoni, walikuwa hamsini na kenda elfu na mia tatu. 24 Katika wana wa Gadi, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 25 wale waliohesabiwa katika kabila ya Gadi, walikuwa arobaini na tano elfu na mia sita na hamsini. 26 Katika wana wa Yuda, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina,
tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 27 wale waliohesabiwa katika kabila ya Yuda, walikuwa sabini na nne elfu na mia sita. 28 Katika wana wa Isakari, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 29 wale waliohesabiwa katika kabila ya Isakari, walikuwa watu hamsini na nne elfu na mia nne. 30 Katika wana wa Zabuloni, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 31 wale waliohesabiwa katika kabila ya Zabuloni, walikuwa hamsini na saba elfu na mia nne. 32 Katika wana wa Yusufu, yaani, wa wana wa Efraimu, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 33 wale waliohesabiwa katika kabila ya Efraimu, walikuwa arobaini elfu na mia tano. 34 Katika wana wa Manase, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 35 wale waliohesabiwa katika kabila ya Manase, walikuwa thelathini na mbili elfu na mia mbili. 36 Katika wana wa Benyamini, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 37 wale waliohesabiwa katika kabila ya Benyamini, walikuwa watu thelathini na tano elfu na mia nne. 38 Katika wana wa Dani, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 39 wale waliohesabiwa katika kabila ya Dani, walikuwa sitini na mbili elfu na mia saba. 40 Katika wana wa Asheri, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 41 wale waliohesabiwa katika kabila ya Asheri, walikuwa arobaini na moja elfu na mia tano. 42 Katika wana wa Naftali, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani; 43 wale waliohesabiwa katika kabila ya Naftali, walikuwa hamsini na tatu elfu na mia nne. 44 Hao ndio waliohesabiwa, ambao Musa na Haruni waliwahesabu, na wakuu wa Israeli, watu kumi na wawili, kila mtu kwa ajili ya nyumba ya baba zake. 45 Hivyo ndivyo walivyokuwa wote waliohesabiwa katika wana wa Israeli, kwa nyumba za baba zao, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani katika Israeli; 46 Hao wote waliohesabiwa walikuwa mia sita na tatu elfu na mia tano na hamsini. 47 Lakini Walawi kwa kabila ya baba zao hawakuhesabiwa miongoni mwao.