Skip to main content

Swahili - The Book of Genesis

Page 1

Mwanzo SURA YA 1 1 Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. 2 Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu; na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi. Na Roho wa Mungu akatulia juu ya uso wa maji. 3 Mungu akasema, Iwe nuru; 4 Mungu akaiona nuru, ya kuwa ni njema; Mungu akatenganisha nuru na giza. 5 Mungu akaiita nuru Mchana, na giza akaliita Usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya kwanza. 6 Mungu akasema, Na liwe anga katikati ya maji, litenge maji na maji. 7 Mungu akalifanya anga, akatenganisha maji yaliyo chini ya anga na maji yaliyo juu ya anga; ikawa hivyo. 8 Mungu akaliita anga Mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili. 9 Mungu akasema, Maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike mahali pamoja, na mahali pakavu paonekane; 10 Mungu akapaita mahali pakavu Nchi; na makusanyo ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. 11 Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; 12 Nchi ikatoa majani, mche utoao mbegu kwa jinsi yake, na mti uzaao matunda, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. 13 Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu. 14 Mungu akasema, Na iwe mianga katika anga ya mbingu ili kutenganisha mchana na usiku; na ziwe kwa ishara, na nyakati, na siku, na miaka; 15 Na iwe mianga katika anga la mbingu itie nuru juu ya nchi; ikawa hivyo. 16 Mungu akafanya mianga miwili mikubwa; mwanga mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku: alizifanya nyota pia. 17 Mungu akaviweka katika anga la mbingu vitie nuru juu ya nchi; 18 na kuitawala mchana na usiku, na kutenganisha nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. 19 Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne. 20 Mungu akasema, Maji na yatoe kwa wingi kiumbe chenye uhai, na ndege waruke juu ya nchi katika anga ya mbingu. 21 Mungu akaumba nyangumi wakubwa, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho, ambavyo maji yalijawa navyo kwa jinsi zao, na kila ndege arukaye kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. 22 Mungu akavibarikia, akisema, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze maji ya baharini, na ndege waongezeke katika nchi. 23 Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tano. 24 Mungu akasema, Nchi na izae kiumbe hai kwa jinsi zake, mnyama wa kufugwa, na kitambaacho, na wanyama wa mwitu kwa jinsi zake; ikawa hivyo. 25 Mungu akafanya mnyama wa mwitu kwa jinsi zake, na mnyama wa kufugwa kwa jinsi zake, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi kwa jinsi yake; na Mungu akaona ya kuwa ni vyema.

26 Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. 27 Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba; mwanamume na mwanamke aliwaumba. 28 Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha, mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. 29 Mungu akasema, Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti ambao matunda yake yana mbegu; itakuwa ni chakula chenu. 30 Na kila mnyama wa nchi, na ndege wa angani, na kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai, nimewapa kila mche wa kijani kuwa chakula; 31 Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita. SURA YA 2 1 Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. 2 Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. 3 Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya. 4 Hivi ndivyo vizazi vya mbingu na dunia vilipoumbwa, siku ile BWANA Mungu alipozifanya mbingu na dunia. 5 Na kila mche wa shambani kabla haujakuwa katika nchi, na kila mche wa shambani kabla haujaota; kwa maana Bwana Mungu alikuwa hajainyeshea nchi mvua, wala hapakuwa na mtu wa kuilima nchi. 6 Lakini ukungu ukapanda kutoka katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa nchi. 7 Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai. 8 Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni; na huko akamweka mtu ambaye amemfanya. 9 Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya. 10 Kukatoka mto katika Edeni wa kuinywesha bustani; na kutoka huko iligawanyika, ikawa vichwa vinne. 11 Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu; 12 Na dhahabu ya nchi hiyo ni nzuri; huko kuna bedola na jiwe la shohamu. 13 Na jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Kushi. 14 Na jina la mto wa tatu ni Hidekeli, ndio upitao upande wa mashariki wa Ashuru. Na mto wa nne ni Eufrate. 15 Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza. 16 Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula; 17 Lakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.


Turn static files into dynamic content formats.

Create a flipbook